Kiongozi wa upinzani Senegal ahukumiwa kifungo cha miaka 5 jela
Mahakama moja nchini Senegal imemhukumu kifungo cha miaka mitano jela Khalifa Sall, kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya ufisadi iliyokuwa ikimkabili.
Meya huyo wa Dakar ambaye anahesabiwa kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa serikali ya Rais Macky Sall, kabla ya hukumu ya leo Ijumaa amekuwa akishikiliwa korokoroni tangu mwaka jana kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma na kugushi vyeti.
Mwanasiasa huyo wa upinzani amekuwa kizuizini kwa madai kuwa aliiba Franca bilioni 1.8 za nchi hiyo, sawa na zaidi ya dola milioni 3.3 za Marekani.
Itakumbukwa kuwa, katika uchaguzi wa Bunge uliofanyika mwezi Julai mwaka jana, muungano wa upinzani unaoongozwa na Khalifa Sall ulishika nafasi ya pili ukifuatiwa na muungano ulioundwa na Abdoulaye Wade, Rais wa zamani wa Senegal.
Muungano tawala unaoungwa mkono na Rais Macky Sall wa nchi hiyo ulifanikiwa kujikusanyia wingi wa kura katika miji 45 ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Ushindi wa muungano huo katika uchaguzi wa Bunge, umemuandalia mazingira Rais Macky Sall ya kutetea kiti chake cha Urais katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwaka ujao wa 2019.