Felix Tshisekedi kuwania urais katika uchaguzi ujao DRC
Chama kikuu cha upinzani nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo UDPS kimemtangaza Felix Tshisekedi kuwa mgombea wake katika uchaguzi mkuu wa rais uliopangwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu.
Akizungumza jijini Kinshasa katika ofisi za chama hicho hii leo, msemaji wa UDPS Peter Kazadi amesema UDPS imeamua kuratibu mapambano yake vizuri kwa kumkabidhi jukumu hilo Felix Tshisekedi Tshilombo kuwania nafasi ya uraisi wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkutano mkuu wa UDPS pia ulimpitisha Tshisekedi kuwa mwenyekiti wa chama hicho baada ya kupata kura 790 kati ya 803 ambayo ni asilimia 98 ya kura zote.
Kwa upande wake Felix Tshisekedi, ambaye sasa anamrithi baba yake Etienne Tshisekedi, aliyefariki dunia tarehe mosi Februari mwaka jana akiwa Ubelgiji, baada ya kutangazwa amesema hatimaye atafanikisha ndoto za waliokuwa waasisi ikiwa uchaguzi utafanyika baadae mwaka huu.
Uchaguzi uliokuwa ufanyike mwaka 2017 mwishoni ulisogezwa mbele na sasa unatarajiwa Desemba 23, 2018 ili kumpata mrithi wa Joseph Kabila, ambaye muhula wake wa uongozi ulitamatika Desemba 20, 2016.
Hayo yametangazwa wakati ambao utafiti mpya wa maoni umeonyesha kuwa, kwa kila raia kumi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wanane hawamungi mkono Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo. Utafiti huo uliofanywa mwezi jana na shirika la utafiti la Congo Research Group CRG likishirikiana na Kituo cha Utafiti wa Maoni cha BERCI katika Chuo Kikuu cha New York unaonyesha wazi kuwa, akthari ya Wakongomani wamechoshwa na uongozi wa miaka 17 wa Rais Kabila na wangetaka kumuona akiachia ngazi.