Hatimaye Miguna Miguna arejeshwa nchini Canada, amlaumu Raila Odinga kwa kumsaliti
Mwanasheria wa upinzani nchini Kenya aliyemuapisha Kinara wa Muungano wa Upinzani (NASA), Raila Odinga kuwa rais wa watu, Miguna Miguna amesafirishwa kwa ndege kutoka mjini Dubai, hadi Toronto, Canada.
Miguna ambaye alikuwa katika uwanja wa ndege wa Dubai kwa muda wa siku nne huku akifuatilia taratibu za kurudi tena nchini Kenya alikofukuzwa, amewasili mjini Toronto mchana wa leo akitumia ndege ya Canada. Awali Jumatatu iliyopita, Miguna alizuiliwa kuingia Kenya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi kutokana na kuwa na pasipoti ya Canada isiyo na visa. Alishindwa kuonesha pasi ya kusafiria ya Kenya na badala yake akaishia kuonyesha kitambulisho pekee cha taifa la Kenya.
Inaelezwa kuwa, pasipoti yake ya Kenya ilichukuliwa mwezi uliopita na polisi ya Kenya na hivyo na kubakia na pasipoti moja ya Canada. Akiwa bado anasubiri taratibu za kuruhusiwa kuingia Kenya kutoka uwanja Jomo Kenyatta, alisafirishwa hadi mjini Dubai bila kujitambua ambapo ilielezwa kuwa, alichomwa sindano ya usingizi na kujikuta yuko Dubai. Hata hivyo Miguna alisisitiza kwamba, hatoenda popote, na badala yake atarudi jijini Nairobi. Wakati hayo yakijiri, Miguna Miguna amemshambulia kiongozi wa NASA Raila Odinga kwa kushindwa kumsaidia kurejea nchini Kenya.
Taarifa aliyoituma Jumamosi kutoka uwanja wa ndege wa Dubai, Miguna alimlaani Odinga kwa kile alichosema kuwa anaendelea kushirikiana na watu ambao huko nyuma alikuwa anadai ni madhalimu. “Raila Odinga hawezi kuendelea kufurahia nje ya nchi pamoja na madhalimu ilhali yule aliyemwapisha kama Rais wa Wananchi, anaendelea kudhulumiwa na watu hao hao walioiba kura zake na kuamuru mauaji ya kinyama dhidi ya wafuasi wake mwenyewe," amesema Miguna. Hadi sasa BRaila Odinga hajatoa taarifa yoyote rasmi kuhusiana na suala hilo la Miguna tangu alipozuiwa kuingia Kenya wiki iliyopita, ingawa Jumatatu iliyopita alifika katika uwanja wa ndege wa JKIA jijini Nairobi katika kile kilichosemekana kuwa ni jaribio la kumsaidia wakili huyo kuingia nchini Kenya.