Hatimae Abiy Ahmed Ali awa rasmi waziri mkuu wa Ethiopia
Abiy Ahmed Ali aliyekuwa anakaimu nafasi ya waziri mkuu wa Ethiopia baada ya maandamano ya wananchi kumlazimisha kujiuzulu waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Hailemariam Desalegn, jana Jumatatu aliapishwa kuwa waziri mkuu rasmi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Abiy Ahmed alikula kiapo jana na hivyo kuwa waziri mkuu wa kwanza Muislamu katika historia nzima ya Ethiopia. Bunge la Ethiopia, jana (Jumatatu) liliitisha kikao cha kumpigia kura Abiy Ahmed na idadi kubwa ya wabunge walimpigia kura ya ndio.
Siku ya Jumanne ya tarehe 27 Machi, 2018, baraza la muungano tawala wa Ethiopia lilikubali ombi la kujiuzulu Hailemariam Desalegn na lilimteua Abiy Ahmed Ali kukaimu nafasi iliyoachwa wazi na waziri mkuu huyo wa zamani wa Ethiopia.
Baraza la muungano tawala wa Ethiopia liliundwa mwaka 1989 na kushirikisha vyama vinne vilivyoundwa kwa misingi ya kikabila na kieneo. Baraza hilo huitisha kikao mwaka mara mbili na katika vikao hivyo ama humbakisha madarakani au huchagua waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.
Tarehe 15 Februari mwaka huu, Hailemariam Desalegn alitangaza ghafla kujiuzulu uwaziri mkuu wa Ethiopia. Baada ya kujiuzulu alisema kuwa, ataendelea kuongoza nchi hiyo hadi baraza la muungano tawala litakapoidhinisha kujiuzulu kwake.
Siku moja baada ya kujiuzulu Desalegn, Baraza la Mawaziri la Ethiopia lilitangaza hali ya hatari nchini humo. Kwa muda mrefu sasa Ethiopia imo katika mgogoro wa kisiasa na maandamano ya wananchi wanaolalamikia utendaji mbovu wa serikali.