Homa ya Lassa imeshaua zaidi ya watu 140 nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42684
Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na homa ya Lassa nchini Nigeria imepindukia 140.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 05, 2018 14:41 UTC
  • Homa ya Lassa imeshaua zaidi ya watu 140 nchini Nigeria

Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na homa ya Lassa nchini Nigeria imepindukia 140.

Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchni Nigeria (NCDC) kimetoa takwimu mpya leo Alkhamisi zinazoonyesha kuwa, tangu Januari mwaka huu hadi sasa, ugonjwa huo umeua watu 142, na kwamba kesi hizo zimerekodiwa katika majimbo 20 kati ya 36 ya nchi hiyo.

Taarifa ya NCDC imesema kuwa, majimbo ya Edo, Ondo na Ebonyi yaliyoko kusini mwa nchi ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na homa hatari ya Lassa.

Ugonjwa wa homa ya Lassa ulishuhudiwa kwa mara ya kwanza nchini Nigeria mwaka 1969 katika mji wa Lasa na kwa sababu hiyo ulipewa jina la mji huo. Ugonjwa huo unashabihiana sana na ule wa Ebola na Marbug.

Dalili za homa ya Lassa

Mwezi Februari mwaka huu, Shirika la Afya Duniani WHO lilitangaza kuwa, homa ya Lassa imeua watu 17 nchini Benin, mbali na kuripotiwa kesi zaidi ya 50 ya ugonjwa huo.

Dalili za ugonjwa huo ambao hukaa mwilini kati ya siku 6 na 21 ni mtu kujisikia mnyonge, baada ya siku chache mgonjwa huanza kuumwa na kichwa, kuwashwa na koo, kuumwa na kifua, kutapika, kuharisha, na kusokotwa na tumbo. Vilevile uso wa mgonjwa  unaweza kufura, kuumwa na mapafu na kutokwa damu mdomoni.