Pezeshkian: Iran iko tayari kwa mwingiliano, lakini haitaacha haki zake za nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128886-pezeshkian_iran_iko_tayari_kwa_mwingiliano_lakini_haitaacha_haki_zake_za_nyuklia
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema Tehran iko tayari kwa mazungumzo kuhusu mpango wake wa amani wa nyuklia lakini kamwe haitaacha haki za taifa hilo.
(last modified 2025-07-28T23:45:12+00:00 )
Jul 28, 2025 23:45 UTC
  • Pezeshkian: Iran iko tayari kwa mwingiliano, lakini haitaacha haki zake za nyuklia

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema Tehran iko tayari kwa mazungumzo kuhusu mpango wake wa amani wa nyuklia lakini kamwe haitaacha haki za taifa hilo.

Pezeshkian aliyasema hayo jana Jumatatu alipokutana na balozi mpya wa Ufaransa mjini Tehran, Pierre Cochard, ambaye aliwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Iran.

"Tunadai haki zetu ndani ya mfumo wa kanuni za kimataifa na kwa kuzingatia matakwa ya mfumo huo," amesema Rais Pezeshkian.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema shughuli za nyuklia za Iran zilikuwa chini ya uangalizi mkali zaidi katika siku za nyuma na kwamba Tehran iko tayari kwa ushirikiano katika suala hili.

"Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba tunafumbia macho haki taifa la Iran. Tuko tayari kwa mazungumzo na hatutafuti vita, lakini majibu yetu kwa uwezekano wowote wa kurudiwa uchokozi yatakuwa yenye nguvu," amesisitiza Rais wa Iran.

Pezeshkian amesema Iran inataka kuwa na maingiliano na dunia, lakini nchi za Magharibi zinavuruga mchakato huu kwa kueneza uongo na kuishutumu Tehran kuwa ifanya juhudi za kutengeneza silaha za nyuklia.

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Rais Pezeshkian amezishutumu nchi za Ulaya hususan Ufaransa kwa kunyamazia kimya jinai "zisizo na kifani na za kikatili" zinazofanywa na utawala wa Israel dhidi ya watu madhulumu wa Palestina huko Gaza.

Watoto wa Gaza wanakufa kwa njaa

Amesema hakuna kinachoweza kuhalalisha kuuawa kwa watu wa Gaza kwa njaa kutokana na mzingiro wa kiuhalifu.

"Je! watoto wachanga wa Gaza ambao wanauawa kwa mabomu au kwa njaa kutokana na kuzingirwa huko Gaza ni magaidi?", amehoji Rais wa Jamhuri ya Kiislamu katika matamshi yake na balozi mpya wa Ufaransa mjini Tehran na kusema: Tunataraji kwamba Ufaransa itakuwa na nafasi kubwa zaidi katika kuzuia jinai za utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina.