Sudan yaishtaki Misri kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan amewasilisha mashtaka ya nchi yake dhidi ya Misri kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya Misri kuendesha uchaguzi wa rais katika maeneo ya mpakani yanayogombaniwa ya Halaib na Shalateen.
Ibrahim Ghandour amesema leo kuwa, hivi karibuni nchi yake imewasilisha mashtaka matatu tofauti kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo mashtaka ya kwanza yanahusiana na kulalamikia kuchorwa mpaka mpya wa majini baina ya Misri na Saudi Arabia baada ya Misri kuipa Saudia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir mwezi Aprili 2016.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan pia amesema mashtaka ya pili ni ya kulalamikia hatua ya Misri ya kujenga bandari mbili za uvuvi katika maeneo ya Shalateen na Aburamad mwezi Februari 2017.
Mashtaka ya tatu kwa mujibu wa waziri huyo yanahusiana na kufanyika uchaguzi wa rais wa Misri katika eneo la mpakani la Halaib linalogombaniwa na nchi hizo mbili.
Tangu mwaka 1958 hadi hivi sasa, Sudan imekuwa ikiwasilisha mashtaka yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kila mwaka kulalamikia vitendo vya Misri katika eneo la Halaib.
Uhusiano wa Misri na Sudan umeharibika sana katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kugombania eneo hilo pamoja na mradi wa Ethiopia wa kujenga bwawa la al Nahdha kwa kutumia maji ya mto Nile. Sudan inaunga mkono mradi huo wa Ethiopia lakini Misri inapinga. Sudan pia inailaumu Misri kuwa inawasaidia waasi wanaopingana na serikali ya Khartoum huko Darfur, magharibi mwa Sudan.