Marekani yapanua uwepo wake wa kijeshi barani Afrika
Marekani imetangaza kuwa inajenga kituo cha ndege zisizo na rubani (drone) za kijeshi nchini Niger kwa shabaha eti ya kukabiliana na makundi ya kigaidi.
Imepangwa kuwa baada ya kukamilika kituo hicho ndege za kivita na ndege zisizo na rubani aina ya MQ-9 za Marekani zilizoko katika mji mkuu wa Niger, Niamey zitahamishiwa katika kituo hicho kipya.
Niger ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye idadi kubwa ya askari wa Marekani. Mauaji ya askari wanne wa Marekani nchini Niger hapo Oktoba mwaka jana yalitumiwa na serikali ya Washington kwa ajili ya kuzidisha uwepo wa majeshi ya nchi hiyo huko Niger. Kwa sasa kuna askari wasiopungua 800 wa Marekani katika nchi hiyo ya Kiafrika. Marekani pia ina kituo cha kijeshi na idadi kubwa ya askari katika nchi ya Djibouti.

Japokuwa askari wa Marekani wamekuwepo kwa miaka mingi katika nchi mbalimbali za Afrika lakini idadi ya akari hao imeongezeka kwa kiwango kikubwa katika nchi za bara hilo katika miaka ya hivi karibuni. Vilevile Marekani inaendelea kujenga na kupanua vituo vya kijeshi katika nchi za Afrika kwa visingizo mbalimbali. Kisingizo kinachotumiwa sasa na maafisa wa serikali ya Marekani kwa ajili ya kujenga na kutuma askari zaidi wa nchi hiyo barani Afrika ni eti kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi kama al Qaida, Daesh na al Shabab.
Mkuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Joseph Dunford anasema: Vita dhidi ya Daesh sasa vinahamia barani Afrika.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kuundwa kwa makundi ya kigaidi kama Daesh na mfano wake katika maeneo mbalimbali kwa hakika ni kisingizio kinachotumiwa na Marekani na washirika wake kwa ajili ya kupanua satua na ushawishi wao wa kisheji katika bara la Afrika.
Kituo cha International Action Center kinasema: "Marekani imezidisha idadi ya askari wake barani Afrika na suala hilo linafanyika sambamba na kuzusha ghasia, machafuko na uharibifu katika baadhi ya nchi za bara hilo. Hivyo kuna udharura wa kukataa na kupinga visingizio vinavyotolewa na Marekani kama vile madai kwamba inapambana na makundi ya kigaidi kama Daesh."

Bara la Afrika lina utajiri mkubwa wa maliasili, nishati, madini, jamii kubwa ya watu na nafasi nzuri ya kijografia na kwa msingi huo madola makubwa ya kikoloni daima yamekuwa yakizikodolea jicho la tamaa nchi za bara hilo. Kwa sasa Afrika imekuwa medani ya ushindani wa madola makubwa yanayowania fursa za kichumi, kisiasa na kibiashara na utajiri wa nchi za Afrika. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, miongoni mwa malengo ya kuzidishwa uwepo mkubwa wa askari wa Marekani katika nchi za Afrika ni kutaka kuzipiku nchi hasimu na wapinzani wa Washington kama Russia na China. La kusikitisha ni kwamba, baadhi ya viongozi na wanasiasa wa Afrika pia wanakaribisha sera hizo za Marekani na kuruhusu kuwepo kambi na vituo vya kijeshi vya Marekani nchini mwao kutokana na kutokomaa kisiasa, matatizo ya kiutawala na kiuchumi na sera za kidikteta na tegeme za wanasiasa wa aina hiyo. Udhaifu huu unatumiwa na Marekani na madola mengine ya kikoloni kwa ajili ya kupanua ushawishi wao wa kisaisa, kiuchumi na kijeshi katika baadhi ya nchi za Afrika na kutimiza malengo yao ya nyuma ya pazia.