Maelfu ya wanawake waandamana DRC kulaani wimbi la mauaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43748-maelfu_ya_wanawake_waandamana_drc_kulaani_wimbi_la_mauaji
Maelfu ya wanawake wamefanya maandamano katika mji wa Beni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kulishinikiza jeshi la nchi hiyo pamoja na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kukabiliana na wimbi la mauaji yanayofanywa na magenge ya waasi katika eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 28, 2018 03:10 UTC
  • Maelfu ya wanawake waandamana DRC kulaani wimbi la mauaji

Maelfu ya wanawake wamefanya maandamano katika mji wa Beni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kulishinikiza jeshi la nchi hiyo pamoja na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kukabiliana na wimbi la mauaji yanayofanywa na magenge ya waasi katika eneo hilo.

Kanali Richard Kazingufu, Kamanda Mkuu wa Polisi mjini Beni amesema wanawake wapatao elfu kumi walioshiriki maandamano hayo jana Ijumaa waliwasilisha malalamiko yao rasmi ya maandishi kwa Meya wa mji huo pamoja na Ofisi ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa, wakitaka hatua za dharura zichuliwe kuzima ukatili huo wa waasi.

Zawadi Masika, Rais wa Jumuiya ya Wanawake mjini Beni amesema wanawake wamejitokeza kwa wingi ili kuonyesha ghadhabu zao kutokana na kuuawa idadi kubwa ya watu katika mji huo.

Magenge ya waasi mashariki mwa DRC yamekuwa yakiwatumia hata watoto wadogo

Ameongeza kuwa, zaidi ya watu 1,500 wameuawa katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Maandamano hayo yamefanyika siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kutangaza habari ya kugundua makaburi mengine matano ya umati katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.