Mafuriko Yazidi kuua Kenya, saba wafariki Rongai
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44038-mafuriko_yazidi_kuua_kenya_saba_wafariki_rongai
Mafuriko yanaendelea kuua watu nchini Kenya ambapo katika tukio la hivi karibuni, watu saba wamefariki dunia katika Kuanti ya Kajiado inayopakana na Nairobi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 04, 2018 08:59 UTC
  • Mafuriko Yazidi kuua Kenya, saba wafariki Rongai

Mafuriko yanaendelea kuua watu nchini Kenya ambapo katika tukio la hivi karibuni, watu saba wamefariki dunia katika Kuanti ya Kajiado inayopakana na Nairobi.

Taarifa zinasema  watu watano wamefariki na wengine 11 wametoweka baada ya kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka daraja la Mto Kandisi  eneo la Ongata Rongai Kaunti ya Kajiado.

Wakaazi wa eneo hilo wanasema waliopoteza maisha walikuwa wakijaribu kuvuka mto huo wakati wa mvua kali zilizosababisha mafuriko Alhamisi jioni. Aidha watu wengine wawili wamepoteza maisha katika mji wa Kiserian katika Kaunti hiyo ya Kajiado.

Kufuatia maafa hayo, idadi ya watu walipoteza maisha kutokana na mvua nchini Kenya tokea mwezi Aprili mwaka huu inakadiriwa kuwa zaidi ya 110 huku wengine zaidi ya laki mbili wakiachwa bila makao.

Helikopta ya Jeshi la Kenya ikiwanusuru walioathirika na mafuriko

Jeshi la Kenya limelazimika kutumia helikopta zake kuwafikishia waathirika misaada na kuwaokoa wale waliokuwa wamekwama maeneo yaliyofurika. Mashirika ya kutoa misaada yanasema mafuriko hayo yameibua maafa ya kibinadamu na kuna haja ya misaada ya dharura. Aidha mafuriko yamepelekea kuibuka kipindupindu katika kauni 15 kati ya kaunti 47 nchini humo. Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya inasema mvua nyingi zitaendelea kushuhudiwa maeneo ya magharibi na kati mwa nchi hiyo huku maeneo mengine yakishuhudia mvua za wastani katika wiki zijazo. Mafuruko pia yameripotiwa katika nchi jirani za Uganda, Tanzania na Somalia.