Afonso Dhlakama, kiongozi wa zamani wa waasi Msumbiji, afariki dunia
Kiongozi wa zamani wa waasi nchini Msumbuji, Afonso Dhlakama, ambaye alikuwa agombee urais mwakani, amefariki dunia Alhamisi akiwa na umri wa miaka 65.
Dhlakama, ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa kundi la waasi la Renamo, alipatikana akiwa amefairki katika mji wa kati wa Gorongosa. Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu sababu za kifo chake.
Rais Filipe Nyusi wa chama tawala cha Frelimo, ambacho kilipigana vita vya muda mrefu na Renamo, ametuma salamu zake za rambirambi na kusema kifo cha Dhlakama kimekuja wakati mbaya Msumbuji.
Rais Nyusi amesema alikuwa na azma ya kushirikiana na Dhlakama kutatua matatizo ya msumbiji. Wafuasi wa Dhlakama hivi karibuni wamepambana na vikosi vya serikali mara kadhaa tangu ashindwe katika uchaguzi miaka minne iliyopita. Dhlakama alitazamiwa kuchuana tena na Rais Nyusi katika uchaguzi wa 2019.
Katika miaka 16 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza punde baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno, watu karibu milioni moja walifariki hadi mwaka 1992, wakati Afonso Dhlakama alisaini makubaliano ya amani na rais wa zamani Joaquim Chissano. Weledi wa mambo wanasema kuna uwezekano wa kuibuka ghasia katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kufuatia kifo cha Dhlakama.