Walioaga dunia baada ya bwawa kuvunja kingo zake nchini Kenya wapindukia 40
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44306-walioaga_dunia_baada_ya_bwawa_kuvunja_kingo_zake_nchini_kenya_wapindukia_40
Watu zaidi ya 40 wamepoteza maisha baada ya bwala la umeme la shirika moja la kibinafsi kuvunja kingo zake katika eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2018 10:16 UTC
  • Walioaga dunia baada ya bwawa kuvunja kingo zake nchini Kenya wapindukia 40

Watu zaidi ya 40 wamepoteza maisha baada ya bwala la umeme la shirika moja la kibinafsi kuvunja kingo zake katika eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya.

Joseph Kioko, Kamanda Mkuu wa Polisi katika mji wa Solai, kaunti ya Nakuru amesema mbali na watu 41 kuthibitishwa kuaga dunia, makumi ya wengine wametoweka na hawajulikana waliko mpaka sasa baada ya kubomoka Bwawa la Patel. 

Nalo Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limetangaza kwenye ukurasa wake rasmi wa Twitter kwamba limefanikiwa kuokoa watu 39.

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kenya, Fred Matiangi amezuru eneo la tukio leo Alkhamisi na kusema kuwa, serikali imeanzisha uchunguzi kutathmini hali ya mabwawa mengine sita katika eneo hilo. 

Maafisa wa MSalaba Mwekundu wakibeba miili za wahanga wa mkasa wa Solai

Kupasuka kwa bwawa hilo usiku wa kuamkia leo kumesababishwa na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha mfululizo mashariki mwa Afrika kwa miezi miwili sasa.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Msalaba Mwekundu, tangu mwezi Machi hadi sasa mvua hizo zimeshaua watu 170 na kusababisha wengine zaidi ya laki mbili kuyahama makazi yao katika kaunti 32 nchini Kenya.