Sheikh Zakzaky hajulikani alipo, njia za mawasiliano zakatwa
Harakati ya Kiislamu Nigeria imeeleza juu ya wasi wasi ilionao kuhusu uwepo wa kiongozi wao, Sheikh Ibrahim Zakzaky, na kubainisha kwamba njia ambazo zilikuwa zikitumiwa na familia na watu wa karibu naye kwa ajili ya mawasiliano zimekatwa.
Ibrahim Musa, Msemaji na Afisa wa Habari wa harakati hiyo amesema nambari ya simu ya rununu iliyokuwa ikitumiwa na watu wa familia ya mwanaharakati huyo wa Kiislamu haiingii tena tangu baada ya kupandishwa kizimbani siku chache zilizopita.
Aidha amesema mawasiliano ya simu ya watu wa familia waliokuwa wanamshughulikia akiwa kizuizini mjini Abuja pia yamekatwa.
Taarifa ya Harakati ya Kiislamu Nigeria imeeleza kuwa, "Maadui wa Sheikh Zakzaky wanapaswa kutambua kuwa, dunia ilishuhudia kiongozi huyo akiwasilishwa mahakamani na hata akiondoka, hivyo Serikali ya Federali ya Nigeria itabeba dhima endapo kitu chochote kibaya kitamfika mwanaharakati huyo."
Hii ni katika hali ambayo, mtoto wa kiume wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Muhammad Ibrahim Zakzaky amesema kuwa, hana taarifa zozote kuhusiana na hali ya baba, mama na kaka zake wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo tangu walipofikishwa mahakama siku chache zilizopita.
Jumanne iliyopita Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe walifikishwa katika Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna katika kile vyombo vya mahakama vilidai ni kikao cha kusikiliza maombi yao ya kuachiwa huru kwa dhamana.
Hata hivyo dakika chache baadaye, kesi hiyo iliakhirishwa hadi Juni 21, na wawili hao wakaripotiwa kurejeshwa mjini Abuja.