Maafisa 40 wa NYS nchini Kenya wakamatwa katika sakata la ufisadi
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametangaza azma madhubuti ya serikali yake ya kupambana na ufisadi.
Rais Kenyatta ameyasema hayo leo akihutubu katika Ikulu ya Nairobi na kuongeza kuwa, "katu hatutawaruhusu watu wasio na maadili. Watu waliopewa majukumu wawe tayari kuhudumia wananchi na sio wao kuhudumiwa."
Rais wa Kenya ameyasema hayo muda mfupi baada ya vyombo vya usalama kuwatia mbaroni makumi ya watu, wanaotuhumiwa kuhusika katika sakata la ufisadi ndani ya Shirika la Huduma kwa Vijana NYS, ambapo karibu Shilingi bilioni 9 (dola milioni 100 za Marekani) zilipotea.
Washukiwa hao wakiwemo Lillian Omollo, Katibu katika Wizara ya Utumishi wa Umma na Vijana na Richard Ndubai, Mkurugenzi wa NYS wanatazamiwa kupandishwa kizimbani kesho Jumanne kujibu mashitaka ya ufisadi wa fedha yanayowakabili.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji amesema ana ushahidi wa kutosha wa kuwafungulia mashtaka watumishi wa umma wapatao 40 na wakurugenzi 24 wa mashirika yanayotuhumiwa kuhusika katika sakata hilo.
Itakumbukwa kuwa, shirika la NYS lilijikuta tena likiandamwa na kashfa ya ufisadi mwaka juzi, ambapo Waziri wa Ugatuzi wa wakati Ann Waiguru alilazimika kujiuzulu kutokana na mashinikizo ya kila upande ya wananchi na viongozi wa upinzani.