Magaidi waua watu 10 kwa kuwakata vichwa nchini Msumbiji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45130-magaidi_waua_watu_10_kwa_kuwakata_vichwa_nchini_msumbiji
Kundi moja la kigaidi limevamia kijiji cha Monjane kaskazini mwa Msumbiji na kuua watu kumi wakiwemo watoto wadogo kwa kuwakata vichwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 29, 2018 13:46 UTC
  • Magaidi waua watu 10 kwa kuwakata vichwa nchini Msumbiji

Kundi moja la kigaidi limevamia kijiji cha Monjane kaskazini mwa Msumbiji na kuua watu kumi wakiwemo watoto wadogo kwa kuwakata vichwa.

David Machimbuko, afisa wa serikali katika kijiji hicho kilichoko mjini Palma, mkoani Cabo Delgado huko kaskazini mwa Msumbiji ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, mmoja wa walengwa wa shambulizi hilo ni chifu wa kijiji cha Monjane, anayedaiwa kuipa polisi taarifa kuhusu maficho ya kundi la kigaidi la al-Shabaab katika misitu ya nchi hiyo.

Hata hivyo polisi ya Msumbiji haijatoa taarifa kuhusu mauaji hayo ya kikatili, lakini baadhi ya duru za habari zinasema yumkini yametekelezwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab. 

Kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda lilikiri kuhusika na mashambulizi ya mwezi Oktoba mwaka jana, dhidi ya kituo cha polisi na kambi ya jeshi katika mji wa Mocimboa da Praia nchini Msumbiji.

Maafisa usalama wakishika doria Msumbiji

Polisi ya Msumbiji ilikabiliana na wapiganaji wa genge hilo waliokuwa na silaha katika mji huo wa bandari wa Mocimboa da Praia katika Bahari ya Hindi ambapo watu 16 waliuawa wakiwemo maafisa wawili wa jeshi la polisi.

Kufuatia hujuma hiyo, Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji aliwapiga kalamu nyekundu Mkuu wa Shirika la Upelelezi na Mkuu wa Majeshi nchini humo.