UN: Migogoro yaifanya robo ya wananchi wa CAR kuwa wakimbizi
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema mapigano na migogoro imeifanya asilimia 25 ya wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.
Takwimu mpya za OCHA zinaonesha kuwa, watu waliofurushwa makwao na kulazimika kuwa wakimbizi wa ndani kufikia mwezi uliopita wa Aprili ni karibu laki 6 na 70 elfu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 70 ikilinganishwa na mwaka jana.
OCHA imesema wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati waliokimbilia usalama wao katika nchi jirani ndani ya muda huo ni zaidi ya laki 5 na 70 elfu.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kwa ujumla watu milioni 1.23 kati ya raia wote milioni 4.5 wa nchi hiyo ya Kiafrika wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.
Hivi karibuni, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) lilieleza wasiwasi lilionao juu ya kumiminika maelfu ya wakimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ni kuwa, kwa wastani wakimbizi wapatao 7,000 kutoka Juamhuri ya Afrika ya Kati huingia Kongo DR kila wiki.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni moja ya nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani Rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka nchini humo.