Jun 06, 2018 07:27 UTC
  • Magaidi wafanya mauaji mengine ya kinyama nchini Msumbiji

Kundi la kigaidi linaloaminika kuwa na mfungamano na al-Shabaab ya Somalia limevamia kijiji kimoja katika mkoa wa Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji na kuua watu saba kwa kuwakata vichwa.

Msemaji wa Polisi nchini humo,  Inacio Dina ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, mbali na kufanya mauaji hayo, genge hilo la kigaidi pia limeteketeza moto nyumba 164 na magari manne katika hujuma hiyo ya jana Jumanne dhidi ya kijiji cha Naude kilichoko wilayani Macomia.

Amesema, na hapa tunanukuu,  "Magaidi hao walitumia mapanga kufanya mauaji hayo. Nadhani kundi hili lina uhusiano na lile lililofanya shambulizi jingine mnamo Mei 27." Mwisho wa kunukuu.

Polisi ya Tanzania na Msumbiji ziliposaini makubaliano ya kuimarisha uhusiano miezi 5 iliyopita

Mei 27, kundi moja la kigaidi lilivamia kijiji cha Monjane kaskazini mwa Msumbiji na kuua watu kumi wakiwemo watoto wadogo kwa kuwakata vichwa. Mmoja wa walengwa wa shambulizi hilo alikuwa ni chifu wa kijiji cha Monjane, aliyedaiwa kuipa polisi taarifa kuhusu maficho ya kundi la kigaidi la al-Shabaab katika misitu ya nchi hiyo.

Kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda lilikiri kuhusika na mashambulizi ya mwezi Oktoba mwaka jana, dhidi ya kituo cha polisi na kambi ya jeshi katika mji wa Mocimboa da Praia nchini Msumbiji, ambapo watu 16 waliuawa wakiwemo maafisa wawili wa jeshi la polisi.

Tags