Watoto milioni 108 duniani wanashiriki kazi zinazohatarisha afya na usalama wao
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani limesema baaada ya miaka mingi ya kupungua, sasa ajira ya watoto katika kilimo imeanza kuongezeka tena ikichochewa na migogoro na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Hayo yalielezwa jana Juni 12 kwa munasaba wa siku ya kupinga ajira kwa watoto duniani ambapo FAO imebaini kuwa mwenendo huu hautishii tu mustakbali wa mamilioni ya watoto, bali pia unatishia juhudi za kutokomeza njaa na umasikini duniani.
Kwa mujibu wa FAO siku ya kupinga ajira kwa watoto duniani mwaka huu imejikita kwa watoto milioni 108 kote duniani wanaoshiriki kazi zinazohatarisha afya na usalama wao, zikiwemo shughuli za uvuvi, kilimo, kukausha samaki kwa moshi na kazi za kuchomelea magari zinazowaweka katika hatari kubwa.
FAO inasema idadi ya watoto walio katika ajira ya kilimo kote duniani imeongezeka kutoka milioni 98 na kufikia milioni 108 mwaka 2012, sababu kuu ikitajwa kuwa ni vita, mabadiliko ya tabia nchi na kulazimishwa kuhama makazi yao.
Taarifa hiyo pia imesema karibu nusu ya watoto wanaolazimishwa ajira katika sekta ya kilimo ni kutoka barani Afrika ambapo idadi hiyo ni milioni 72 huku bara Asia likiwa ni la pili kwa idadi ya milioni 62.
Jacqueline Demeranville afisa wa FAO anayehusika na ajira vijijini anasema ushirikishaji wa watoto katika kazi zenye madhara ni ukiukwaji dhahiri wa haki zao. Aidha amesemaa kuna athari za muda mrefu za mustakhbali wa watoto wanahudumu katika kazi za kilimo huku akibiani kuwa ajali moja tu inaweza kusambaratisha uwezekano wa kipato katika maisha yao yote.