Ethiopia kuwasamehe mamia ya watu waliohukumiwa kwa makosa ya ugaidi
Serikali ya Ethiopia imesema kuwa itawafutia mashtaka zaidi ya wafungwa 304 wakiwemo 289 wanaotumikia vifungo vya makosa ya ugaidi.
Hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni sehemu ya kasi kubwa ya marekebisho yanayofanywa na serikali mpya ya nchi hiyo baada ya kutokea machafuko miaka mitatu iliyopita.
Machafuko hayo yalienea haraka katika maeneo yote ya Ethiopia yakitaka uhuru zaidi wa kisiasa na uadilifu, sambamba na kukomeshwa uvunjaji wa haki za binadamu. Maandamano hayo hatimaye yalimlazimisha waziri mkuu wa zamani wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn ajiuzulu na nafasi yake kuchukuliwa na Abiy Ahmed mwezi Aprili mwaka huu.
Msamaha uliotolewa jana Ijumaa unawahusu pia raia watatu wa Kenya ambao wameachiliwa huru kwa mujibu wa maafikiano ya nchi mbili ya kuimarisha uhusiano wao.
Zaidi ya wafungwa 1,000 wameshaachiliwa huru au wako mbioni kuachiliwa huru tangu Waziri Mkuu Abiy Ahmed achukue madaraka ya Ethiopia mwezi Aprili.
Miongoni mwa walioachiliwa huru katika miezi ya hivi karibuni ni viongozi wa ngazi za juu wa upinzani waliofungwa jela kwa tuhuma za ugaidi au kufanya njama za kuipindua serikali.
Mmoja wa viongozi hao waandamizi wa upinzani ni baba wa watoto watatu, Andargachew Tsige aliyepatikana na hatia ya ugaidi na kuhukumiwa kifungo jela mwaka 2009 akiwa hayupo mahakamani. Alipatikana pia na hatia ya kuhusika na kundi la upinzani la Ginbor 7. Tsige alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Yemen mwaka 2014 na kurejeshwa nchini Ethiopia kutumikia kifungo chake, kabla ya waziri mkuu mpya wa nchi hiyo kumfutia makosa na kumtoa jela.