Maafisa wanane wa polisi wa Kenya wauawa katika Kaunti ya Wajir
Maafisa wasiopungua wanane wa polisi wameuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu katika eneo la Bojigaras, kwenye Kaunti ya Wajir huko kaskazini mashariki mwa Kenya.
Jeshi la Polisi la Kenya limesema kuwa, gari walilokuwa wanasafiria maafisa hao lilikanyaga kifaa cha mripuko na kurushwa juu jana Jumapili. Watu walioshuhudia wamesema kuwa gari hilo limeharibiwa vibaya na kuua watu waliokuwemo.
Muhammad Saleh, mratibu wa eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya amesema, waliofanya shambulizi hilo wametoweka mara moja na kuongeza kuwa, uchunguzi wa awali unaonesha kuhusika genge la kigaidi la al Shabab la nchini Somalia. "Waliofanya shambulizi hilo wametoweka mara baada ya mripuko huo na tunashuku al Shabab ndio waliohusika," amesema.

Askari wa kuongeza nguvu wametumwa haraka kwenye eneo hilo. Shambulizi hilo limetokea baada ya kutolewa tahadhari kadhaa za uwezekano wa kutokea mashambulizi ya genge hilo la kigaidi. Maafisa usalama walitahadharisha wiki iliyopita kuwa magaidi wanapanga kufanya mashambulizi kabla ya kumalizika mwezi wa Ramadhani.
Katika upande mwingine, msemaji wa jeshi la polisi la Kenya Charles Owino amesema kuwa mashirika ya usalama yamepata taarifa za kuaminika zinazosema kuwa magaidi wa al Shababu wamepanga kufanya mashambulizi katika maeneo tofauti ya Kenya wakati huu wa Fainali za Kombe la Dunia la mpira wa miguu na baada ya mwezi wa Ramadhani. Vilevile amewataka Wakenya kuchukua tahadhari zaidi hasa wanapokuwa katika maeneo ya watu wengi kama mahotelini, kwenye vituo vya mabasi, mashuleni n.k, wakati huu wa Fainali za Kombe la Dunia za mpira wa miguu zinazoendelea nchini Russia.