Misri yachukua hatua kali za usalama kukabiliana na malalamiko ya wananchi
Serikali ya Misri imechukua hatua kali za kiusalama kwa ajili ya kukabiliana na malalamiko ya wananchi baada ya kuzidishwa bei ya nishati nchini humo.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imetangaza kuwa, imezidisha idadi ya askari usalama katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo hususan kwenye vituo vya petroli kwa ajili ya kudhibiti upinzani na malalamiko ya wananchi.
Ripoti zinasema kuwa, malalamiko ya wananchi kupinga ongezeko la bei ya mafuta ya petroli yameenea kote nchini Misri na raia wa nchi hiyo wanasema hatua hiyo ya serikali ya Rais Abdel Fattah al Sisi inazidisha mashinikizo kwa tabaka lenye kipato cha chini.
Kwa mara ya pili, serikali ya Misri ilizidisha bei ya mafuta na nishati kwa ujumla katika siku ya pili ya sikukuu ya Idul Fitri kwa asilimia 17 hadi 66, kwa mujibu wa mapatano yake na Mfumko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), suala ambalo limewashtua na kuwakasirisha raia wa nchi hiyo.
Hii ni mara ya pili kwa serikali ya al Sisi kupandisha bei ya nishati tangu mwezi Novemba mwaka 2016.