Watu 75 waripotiwa kupoteza maisha kwa ugonjwa wa kipindupindu nchini Kenya
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya nchini Kenya imesema kuwa, jumla ya watu 75 wamepoteza maisha kwa ugonjwa wa kipindupindu tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Wizara ya Afya ya Kenya imeongeza kuwa, kutokana na ongezeko la magonjwa ya kuambukiza kama vile kipindupindu, surua na homa ya Chikungunya lililoripotiwa katika kaunti 19, hadi sasa watu 4,954 wamekumbwa na ugonjwa thakili wa kipindupindu tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2018. Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Wizara ya Afya ya Kenya, serikali imetuma timu maalumu katika kaunti zilizoathirika na maradhi hayo kwa ajili ya kuzuia ongezeko lake.
Itakumbukwa kuwa, mwanzoni mwa mwaka huu serikali za Tanzania na Kenya zilitangaza kwamba ziko mbioni kudhibiti ugonjwa wa Homa ya Chikungunya unaoambukizwa na mbu aina ya aedes; ugonjwa huo hauna kinga wala tiba mahsusi. Aidha miezi kadhaa iliyopita serikali ya Kenya ilichukua hatua za kufunga hoteli na migahawa kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao hadi wakati huo ulikuwa umesababisha vifo vya watu kadhaa.