Ripoti: Mashambulizi ya 'kigaidi' Msumbiji yameua watu 39 tangu Mei
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kwa akali watu 39 wameuawa katika mashambulizi yanayoaminika kuwa ya kigaidi huko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Mei mwaka huu hadi sasa.
Akizungumza wakati wa kutoa ripoti ya shirika hilo jana Jumanne, Dewa Mavhinga, Mkurugenzi wa Human Rights Watch eneo la kusini mwa Afrika amesema Juni 5, magaidi hao walichoma moto msikiti na kumkata kichwa kiongozi mmoja wa Kiislamu katika kijiji kimoja kilichoko mkoani Cabo Delgado.
Amesema kwa mujibu wa uchunguzi wao, watu wasiopungua 39 wameuawa huku wengine zaidi ya elfu moja wakilazimika kuyahama makazi yao wakihofia usalama wao katika mkoa huo, tokea mwezi uliopita wa Mei hadi sasa.
Mapema mwezi huu, kundi la kigaidi la Al-Sunna wa Jama’a linaloaminika kuwa na mfungamano na al-Shabaab ya Somalia lilivamia kijiji kimoja katika mkoa wa Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji na kuua watu saba kwa kuwakata vichwa, mbali na kuteketeza moto nyumba 164 na magari manne katika hujuma hiyo dhidi ya kijiji cha Naude kilichoko wilayani Macomia.
Aidha Mei 27, kundi hilo lilivamia kijiji cha Monjane kaskazini mwa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika na kuua watu kumi wakiwemo watoto wadogo kwa kuwakata vichwa.
Kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda lilikiri kuhusika na mashambulizi ya mwezi Oktoba mwaka jana, dhidi ya kituo cha polisi na kambi ya jeshi katika mji wa Mocimboa da Praia nchini Msumbiji, ambapo watu 16 waliuawa wakiwemo maafisa wawili wa jeshi la polisi.