Nchi za kaskazini mwa Afrika zagoma kuwapokea wahajiri wa Kiafrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46457-nchi_za_kaskazini_mwa_afrika_zagoma_kuwapokea_wahajiri_wa_kiafrika
Nchi tano za kaskazini mwa Afrika zimekataa mapendekezo ya viongozi wa Ulaya ya kuanzisha kambi maalumu za wahajiri katika ardhi za nchi hizo kwa ajili ya kuwapokea wahajiri wa Kiafrika.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 30, 2018 07:31 UTC
  • Nchi za kaskazini mwa Afrika zagoma kuwapokea wahajiri wa Kiafrika

Nchi tano za kaskazini mwa Afrika zimekataa mapendekezo ya viongozi wa Ulaya ya kuanzisha kambi maalumu za wahajiri katika ardhi za nchi hizo kwa ajili ya kuwapokea wahajiri wa Kiafrika.

Nchi hizo tano za kaskazini mwa Afrika ambazo ni Misri, Tunisia, Libya, Algeria na Mauritania zimetangaza kuwa, zinapinga mpango huo wa Umoja wa Ulaya. Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya jana walifikia makubaliano huko Brussels Ubelgiji kuhusiana na mgogoro wa wahajiri ambapo kwa mujibu wa makubaliano hayo, wahajiri wa Kiafrika walioko katika nchi za Ulaya watahamishiwa katika nchi za kaskazini mwa Afrika.

Hata hivyo viongozi wa nchi ambazo Umoja wa Ulaya umeziainisha kama chaguo lao la kuwahamishia wahajiri hao, wametangaza kupinga vikali mpango huo. Taarifa ya nchi hizo iliyotolewa kwa nyakati tofauti inaeleza kuwa, zinapinga kuanzishwa kambi za wahajiri wa Kiafrika katika ardhi ya nchi zao.

Wahajiri wa Kiafrika wakiwa katika Bahari ya Mediterenia

Wakati huo huo, Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imelaani makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Ulaya kuhusu sera za jinsi ya kuamiliana na wahajiri wanaoelekea barani Ulaya, ambapo makubaliano hayo yamejikita katika kuzuia wahajiri kuingia barani Ulaya na kulaani operesheni za kuwaokoa wakimbizi na wahamiaji.

Licha ya kuwa, idadi ya wakimbizi wanaoelekea Ulaya imepungua kwa kiasi fulani, lakini bado maelfu ya wahajiri na wakimbizi wanapanda mawimbi ya bahari ya Mediterrania kuelekea barani humo lengo likiwa ni kwenda kutafuta maisha mazuri.