Jul 02, 2018 07:38 UTC
  • Boko Haram yaendeleza ukatili, yaua askari wengine 10 Niger

Askari kumi wa Niger wameuawa katika hujuma mpya ya Boko Haram kusini mashariki mwa nchi, karibu na mpaka na Nigeria.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Niger, Abdoul-Aziz Toure ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, shambulizi hilo la jana Jumapili lilifanyika katika kijiji cha Bla Brin, yapata kilomita 40 kutoka mji wa N'Guigmi, karibu na eneo la Ziwa Chad, ambapo wapiganaji wa Boko Haram walishambulia ngome za askari hao.

Amesema askari kumi wamethibitisha kupoteza maisha, huku wengine wanne wakitoweka, isijulikane iwapo walitekwa nyara na wanachama wa genge hilo la ukufurishaji au la.

Juzi Jumamosi, magaidi wa kundi la Boko Haram walishambulia kambi ya wakimbizi wa ndani ya nchi,  katika hujuma waliyotekeleza katika eneo la mpaka wa Nigeria na Cameroon ambapo watu wasiopungua wanne waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Wapiganaji wa Boko Haram

Mapema mwezi jana wa Juni, watu tisa waliuawa katika mashambulio kadhaa ya mabomu huko kusini mashariki mwa Niger karibu na mpaka wa nchi hiyo na Nigeria, hujuma zinazoaminika kufanywa na Boko Haram.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

Tags