Mashirika ya kutetea haki za binadamu yaitaka Ufaransa iache kuiuzia silaha Misri
Mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu yameitaka serikali ya Ufaransa kusimamisha uuzaji wa silaha kwa Misri, yakisisitiza kuwa silaha hizo zinatumiwa na vyombo vya usalama kuwanyamazisha na kuwawekea mbinyo wapinzani na wakosoaji wa serikali.
Mashirika manne ya kutetea haki za binadamu yakiongozwa na International Federation for Human Rights yenye makao yake mjini Paris, yameitaka Ufaransa kusimamisha mauzo ya silaha, mifumo ya kijasusi, magari ya deraya, ndege za kivita na manowari kwa serikali ya Misri, yakisisitiza kuwa silaha hizo zinazotumiwa vibaya na serikali dhidi ya wapinzani.
Aidha yamelitaka Bunge la Ufaransa kuanzisha uchunguzi kuhusu kampuni za serikali na za kibinafsi zinazoiuzia serikali ya Cairo silaha hizo.
Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International pia limewahi kutoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuacha mara moja mauzo ya silaha kwa Misri kutokana rekodi za ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Amnesty ilisema takribani nusu ya nchi wanachama wa EU zimepuuza mwito wa kusitisha uuzaji wa silaha nchini Misri na hivyo kusababisha hatari ya wimbi la mauaji ya kiholela, watu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha mikokoni mwa vyombo vya usalama na ukandamizaji.
Kwa mujibu wa takwimu za Amnesty, nchi 12 kati ya 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya zinasalia kuwa wasambazaji wakubwa wa silaha na suhula nyingine kwa ajili ya jeshi na polisi ya Misri.