Washukiwa wawili watiwa nguvuni kuhusiana na mlipuko wa Zimbabwe
Polisi nchini Zimbabwe imewatia mbaroni washukiwa wawili kuhusiana na mlipuko wa guruneti ulioua watu wawili na kuwajeruhi wengine 47 katika mkutano wa kampeni wa Rais Emmerson Mnangagwa mwezi uliopita.
Mnangagwa ambaye alichukua nafasi ya kiongozi mkongwe wa Zimbabwe, Robert Mugabe kupitia mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu mwezi Novemba mwaka jana amesema kuwa anashuku kwamba wapinzani ndani ya chama chake ndio waliohusika na kile alichokitaja kuwa ni jaribio la kutaka kumuua katika mji wa Bulawayo kusini mashariki mwa Zimbabwe.
Godwin Matanga Kamishna Mkuu wa Polisi ya Zimbabwe amesema kuwa washukiwa wawili wameshatiwa nguvuni na wanaendelea kuwasaka wengine. Amesema wanaendelea kuomba kupewa taarifa zaidi ambazo zinaweza kuwasaidia kuwakamata wale wote waliohusika katika kitendo hicho cha kinyama.
Akizungumza na shirika la utangazaji la BBC mwezi uliopita, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabe alibainisha kuwa anaamini kuwa shambulio hilo lilitekelezwa na kundi la G-40; tawi lilipo ndani ya chama tawala cha ZANU-PF ambalo lilitaka Mugabe arithiwe uongozi na mkewe Grace. Hata hivyo Rais Mnangagwa hakumtuhumu Grace Mugabe kuwa amehusika kivyovyote katika shambulio hilo dhidi yake.