Afrika Kusini yasema itaendelea kulaani jinai za Israel huko Palestina
Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kuwa mashambulizi yanayoendelea kufanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina hususan katika Ukanda wa Gaza hayakubaliki na kwamba kwa sababu hiyo balozi wake hatarejea Tel Aviv.
Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Lindiwe Sisulu amesema nchi yake haiwezi kunyamaza kimya kuhusu hali ya Wapalestina na kwa msingi huo balozi wa Pretoria hatarudi tena katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.
Sisulu ameongeza kuwa, Afrika Kusini haitatuma balozi huko Israel hadi pale hali ya Ukanda wa Gaza itakapoboreka na kusitishwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni.
Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini amesema mashambulizi yanayofanywa na Israel dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na kwamba nchi yake haiwezi kufumbia macho uhalifu huo.
Mwezi Mei mwaka huu Afrika Kusini ilimrejesha nyumbani balozi wake mjini Tel Aviv ikilalamikia mauaji yaliyofanywa na askari wa Israel huko Palestina hususan katika mpaka wa Ukanda wa Gaza.
Tarehe 30 Machi maelfu ya Wapalestina walianza maandamano ya amani ya kuadhimisha Siku ya Ardhi yalityopewa jina la Haki ya Kurejea Nyumbani na hadi sasa askari wa Israel wameua shahidi raia wasiopungua 145 wa Kipalestina na kujeruhi wengine zaidi ya 15 elfu na 500.