Iran na Ivory Coast kuimarisha uhusiano wa pande mbili
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46678-iran_na_ivory_coast_kuimarisha_uhusiano_wa_pande_mbili
Balozi wa Iran nchini Ivory Coast amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili hizi hususan katika nyuga za diplomasia na siasa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 10, 2018 07:06 UTC
  • Iran na Ivory Coast kuimarisha uhusiano wa pande mbili

Balozi wa Iran nchini Ivory Coast amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili hizi hususan katika nyuga za diplomasia na siasa.

Shakib-Mehr, Balozi wa Iran mjini Abidjan ameyasema hayo katika mkutano wake na Guillaume Soro, Spika wa Bunge la Ivory Coast na kubainisha kuwa, kikao chao hicho ni muendelezo wa jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kibunge wa nchi mbili.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amegusia ujumbe wa Spika wa Majilisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran), unaoisisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano na ushirikiano miongoni mwa wabunge wa Iran na Kodivaa.

Kadhalika wawili hao wamesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili za Iran na Ivory Coast, haswa kwa Jamhuri ya Kiislamu kuipa uzoefu na kuisaidia nchi hiyo ya Kiafrika katika nyuga za uchukuzi, biashara na elimu.

Naibu Spika wa Kodivaa alipokutana na Dkt Larijani mjini Tehran

Mapema mwaka huu, Spika wa Bunge la Iran Dakta Ali Larijani alikutana na Privat Oula, Naibu Spika wa Bunge la Ivory Coast hapa mjini Tehran pambizoni mwa Mkutano wa 13 wa Mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Kiislamu.

Naibu Spika huyo wa Kodivaa alisisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa nchi yake na Iran katika nyuga za uchumi na mabunge, huku akimualika Dakta Larijani aitembelee nchi yake.