Jul 11, 2018 13:27 UTC
  • Raia 232 wameuawa Sudan Kusini miezi miwili iliyopita

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limesema raia 232 wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa katika maeneo ya Mayendit na Leer nchini Sudan Kusini.

Taarifa ya baraza hilo imesema mashambulizi hayo ya kati ya Aprili, 16 na Mei, 24 yalitekelezwa na watu binafsi wanaofungamana na serikali ya Sudan Kusini, vikosi vinavyoiunga mkono serikali na vijana wenye silaha wanaotoka maeneo yanayodhibitiwa na wapinzani

Baraza hilo limesema katika ripoti yake kuwa uchunguzi umetambua kwamba watu watatu wanaotuhumiwa kuwa watekelezaji wakuu wa mauaji hayo, mmoja wao ameripotiwa kuondolewa kwenye nafasi yake kwa tuhuma za kujihusisha na matukio hayo.

Kamishna mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Bw. Zeid Ra'ad Al Hussein ameitaka serikali isimamishe mashambulizi yote dhidi ya raia, kuanzisha uchunguzi na kuwachukulia hatua wahalifu wakiwemo wale wanaowajibika kutoa amri.

Watoto w Sudan Kusini wanaolazimishwa kuhudumu kama askari

Hayo yanaripotiwa siku chache baada ya mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF kutangaza kuwa, watoto watatu kati ya wanne huko Sudan Kusini hawana wanachofahamu isipokuwa vita.

Takwimu zinaonyesha kuwa, watoto milioni 2.6 nchini Sudan Kusini wamezaliwa wakati wa vita vilivyoibuka mwaka 2013, ikiwa ni miaka miwili tu tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mwaka 2011.

 

Tags