Jul 14, 2018 07:47 UTC
  • Baraza la Usalama la UN lataka kusitishwa mapigano CAR

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine limetoa wito wa kusitishwa mapigano ya ndani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Taarifa iliyotolewa jana na Baraza la Usalama mjini New York imeeleza wasiwasi wa wanachama wa baraza hilo kuhusu mashambulizi yanayoendelea kufanywa na makundi ya waasi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui na maeneo mengine ya nchi hiyo na kutangaza kuwa, inalaani mashambulizi yote yanayofanywa dhidi ya raia, askari wa kulinda amani na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu ambayo yanaua na kujeruhi idadi kubwa ya watu.

Taarifa hiyo pia imesema kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linayataka makundi yote yanayobeba silaha mjini Bangui na maeneo mengine ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kukomesha ukatili na kukabidhi silaha zao na kujiunga na mchakato wa kurejesha amani nchini humo bila ya masharti yoyote. 

Ghasia na mapigano yanaendelea Bangui

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limesisitiza tena uungaji mkono wake kwa Rais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na limewataka maafisa wa serikali, viongozi wa Umoja wa Afrika na nchi za eneo hilo kuzidisha juhudi za kupatikana mapatano ya kitaifa nchini humo. 

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika vita na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013, na makundi mbalimbali ya waasi yamekuwa wakipigana mara kwa mara yakigombania maeneo yenye utajiri wa madini ya almasi na dhahabu.  

Tags