Bunge la Misri lapasisha sheria inayowapa kinga majenerali wa jeshi
(last modified Tue, 17 Jul 2018 02:55:21 GMT )
Jul 17, 2018 02:55 UTC
  • Bunge la Misri lapasisha sheria inayowapa kinga majenerali wa jeshi

Bunge la Misri Jumatatu ya jana lilipasisha sheria inayowapa kinga ya kufikishwa mahakamani majenerali wa jeshi wanaohusishwa na machafuko yaliyotokea baada ya mapinduzi ya Rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia nchini humo. Maelfu ya raia wa Misri walimiminika mitaani kupinga mapinduzi ya jeshi yaliyomuondoa madarakani Mohamed Mursi.

Sheria hiyo inampa Rais Abdel Fattah al-Sisi haki ya kuteua majenerali wanaopaswa kupewa tuzo na kinga ya kufikishwa mahakamani kutokana na uhalifu liofanyika kuanzia Julai 3 mwaka 2013 hadi tarehe 8 Juni 2014, kipindi ambacho rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia wa Misri, Mohamed Mursi aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya jeshi.

Mamia ya raia waliuawa wakati askari usalama wa serikali ya Cairo walipovamia Medani ya Rabia mjini Cairo Agosti mwaka 2013.

Mamia ya raia waliuawa Rabia, Cairo

Awali Msemaji wa harakati ya Ikhwanul Muslimin nchini Misri alikosoa hatua ya serikali ya Jenerali Abdel Fattah al-Sisi ya kuimarisha nafasi ya wanajeshi nchini humo na mwafaka wa Bunge wa kuwapa kinga ya sheria makamanda wa jeshi la nchi hiyo.

Talat Fahmi amepinga suala la kuwapa kinga ya sheria makamanda wa jeshi la Misri na kusema: Sheria hii ina maana ya kudumisha uhalifu wa wanajeshi ambao miaka mitano iliyopita walifanya mapinduzi dhidi ya serikali halali na vilevile inahalalisha jinai hiyo na kuwapa kinga makatili na wauaji.

Zaidi ya raia elfu moja waliuawa kwa kupigwa risasi wakati askari usalama wa serikali ya Cairo walipovamia maandamano ya amani katika Medani ya Rabia al Adawiyya na mengine katika eneo la Giza.

Tags