Jul 21, 2018 01:18 UTC
  • HRW: Serikali na wanaotaka kujitenga wamehusika na jinai Cameroon

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema jeshi la serikali na kundi linalotaka kujitenga eneo la watu wanaozungumza Kiingereza Cameroon wamehusika katika mauaji na jinai nyingine za kutisha nchini humo.

Mausi Segun, Mkurugenzi wa Human Rights Watch kanda ya Afrika amesema mgogoro wa Cameroon umefikiwa kiwango cha kutia wasiwasi. Ripoti mpya ya shirika hilo imesema zaidi ya watu 180,000 wamelazimika kuyaacha makazi yao katika maeneo yanayozungumza lugha ya Kiingereza, kusini magharibi mwa Cameroon na kukimbilia eneo la wazungumzaji wa Kifaransa tangu Disemba mwaka jana hadi sasa. 

Ikitoa radiamali yake kwa ripoti hiyo, serikali imekiri kwamba imewakamata watu 965 tangu mgogoro huo uanze mwaka 2016, ambapo 114 miongoni mwao wamehukumiwa vifungo mbalimbali huku 30 wakiachiwa huru.

Maeneo ya kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa Cameroon ni ya wakazi wanaozungumza lugha ya Kiingereza na wanaunda asilimia 20 ya wakazi wote wa nchi hiyo.

Kundi la watu wanaotaka eneo lao lijitenga na Cameroon

Takwimu zinaonesha kuwa, tangu mwishoni mwa mwaka jana 2017 hadi hivi sasa, askari karibu 30 wa serikali wameuawa katika mashambulizi ya watu wanaotaka kujitenga na kujitangazia nchi yao huko kusini magharibi mwa Cameroon.

Aidha makumi ya raia wameripotiwa kuuawa katika ghasia hizo.

Tags