Magaidi 13 waangamizwa na polisi ya Misri Peninsula ya Sinai
Jeshi la Polisi la Misri limetangaza habari ya kuua wanachama 13 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika eneo la Sinai, kaskazini mwa nchi.
Duru za habari kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri zimearifu kuwa, maafisa wa polisi walivamia sehemu walikokuwa wamejificha magaidi hao katika mji wa al-Arish, baada ya kudokezwa na wakazi wa mji huo.
Hata hivyo duru hizo za habari hazijatoa maelezo yoyote kuhusu iwapo maafisa usalama wa Misri wameuawa au kujeruhiwa katika makabiliano hayo.
Habari zaidi zinasema kuwa, magaidi hao wameuawa katika ufyatulianaji risasi na maafisa usalama wa Misri.
Mapema mwezi huu maafisa usalama wa Misri walishambulia maficho ya magaidi hao wakufurishaji katika mji wa al-Arish na kuangamiza magaidi wengine 11.
Itakumbukwa kuwa, Februari mwaka huu, jeshi la Misri kwa kushirikiana na polisi lilianzisha operesheni ya pamoja inayojulikana kwa jina la 'Sinai 2018' kwa shabaha ya kuyasafisha magenge ya kigaidi katika eneo hilo la kaskazini mwa nchi.
Duru za habari zimeeleza kuwa, magaidi wasiopungua 280 wameshauawa tangu ilipoanza operesheni hiyo na watu 4467 wameshatiwa mbaroni. Kadhalika jeshi la Misri limepoteza askari wake karibu 40 katika operesheni hiyo.