Makamu wa zamani wa rais wa Kenya awashangaza watu mahakamani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47766-makamu_wa_zamani_wa_rais_wa_kenya_awashangaza_watu_mahakamani
Makamu wa zamani wa rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka, leo amewashangaza Wakenya baada ya kuonekana mahakamani alikokwenda kushiriki katika utetezi wa Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Aug 29, 2018 10:45 UTC
  • Makamu wa zamani wa rais wa Kenya awashangaza watu mahakamani

Makamu wa zamani wa rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka, leo amewashangaza Wakenya baada ya kuonekana mahakamani alikokwenda kushiriki katika utetezi wa Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu.

Kalonzo ambaye kiutaalamu ni wakili, hajawahi kushiriki katika utetezi wa kesi yoyote kama wakili kwa miaka mingi sasa bali zaidi amekuwa akijishughulisha na masuala ya siasa na ya familia yake.

Makamu huyo wa zamani wa Kenya ambaye ana shahada ya uzamili (master degree) ya sheria, ameshiriki katika utetezi wa kesi ya Naibu Jaji Mkuu, Pholomena Mwilu na mahakama imeamrisha kusimamishwa kwa muda kesi hiyo.

Makamu wa zamani wa rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka akionekana mahakamani kumtetea Naibu Jaji Mkuu, Pholomena Mwilu

 

Huo unaonekana ni ushindi kwa Kalonzo na wenzake na ni pigo kwa mwendesha mashtaka mkuu wa Kenya, Noordin Haji ambaye alifungua kesi mahakamani ya kumshitaki Mwilu na wakili Stanley Kiima kwa madai ya ufisadi.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao ni wizi, kutumia vibaya nafasi zao za kazi pamoja na kushindwa kulipa kodi kulikopelekea kufilisika benki ya Imperial.

Akitoa hukumu hiyo, Jaji Chacha Mwita amesema, kuna masuala ya kikatiba inabidi yaunganishwe kwenye shauri hilo hasa kwa kuzingatia kuwa kesi hiyo inahusiana na masuala ya fedha na biashara baina ya mtu binafsi na benki, hivyo katiba lazima itoe ufafanuzi iwapo je jambo hilo linaweza kupelekea kukamatwa jaji huyo au la.

Mahakama hiyo imesimamisha kesi hiyo kutokana na kuhusika kwake na masuala la kikatiba ambayo inabidi yatoe ufafanuzi kuhusu hududi za sheria. Kesi hiyo itasikilizwa tena Oktoba 9, mwaka huu.