Aug 31, 2018 06:34 UTC
  • WFP yatoa msaada wa dharura wa chakula kwa waathirika wa Ebola DRC

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limeanza kutekeleza mpango wa dharura wa kugawa chakula kwa waathirika wa ugonjwa wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Katika taarifa yake iliyotolewa Goma, mashariki mwa DRC, WFP inasema, wanashirikiana na shirika la kimataifa la utoaji misaada la Caritas kugawa chakula kwa wagonjwa na pia watu wengine ambao wamethiriwa kwa njia moja au nyingine na mlipuko huo katika maeneo ya Kivu Kaskazini.

Kwa mujibu wa mkuu wa Ofisi ya WFP nchini DRC, Claude Jibir, mlipuko huo wa 10 wa Ebola umetokea katika eneo ambalo limegubikwa na vita. WFP hivi sasa ,inapanua wigo wa huduma zake zake na kuwahusisha waathirika wa Ebola  kwani hapo kabla ilikuwa ikiwasaidia zaidi maelfu ya watu walioathiriwa na vita katika mkoa huo ambapo katika kitovu cha mlipuko wa Ebola eneo la Beni, watu 12,000 wasio na makazi  wamekuwa wakisaidiwa na WFP kwa kupewa chakula tangu  mwezi Julai.

Mgonjwa wa Ebola akipatiwa msaada 

Watu takriban 4,000 hupokea msaada wa chakula  cha kuwatosheleza kwa mwezi mmoja ikiwemo nafaka, maharage, mafuta ya kupikia,na chumvi na kwa wagonjwa wa Ebola huwa wanapewa biskuti zinazoongeza nguvu.

Tangu ulipozuka upya ugonjwa wa Ebola hadi hivi sasa, kumesharipoti kesi 111 za ugonjwa hukok huko DRC,  huku kesi 83 zikithibitishwa ni za ugonjwa huo na watu zaidi ya 4,000 wamepewa chanjo huku kwa akali 63 wakipoteza maisha.

Tags