Wakenya wamshambulia Seneta aliyemtetea Mchina aliyetoa matusi machafu dhidi yao
Wananchi wa Kenya wamemshambulia vikali katika mitandao ya kijamii seneta wa eneo la Elgeyo, Marakwet Kipchumba Murkomen kutokana kauli yake aliyoitoa kufuatia sakata la kutiwa mbaroni raia wa China kwa jina Liu Jiaqi aliyewatusi Wakenya pamoja na Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwaita nyani.
Seneta Murkomen ambaye ni kiongozi wa walio wengi katika bunge la seneti alishambuliwa baada ya kukosoa hasira za Wakenya kwa kuandika kuwa, kuna Wakenya ambao hutoa matusi mabaya hata kuliko ya Liu Jiaqi. Mchina huyo ambaye alikuwa akijishughulisha na biashara ya kuuza pikipiki katika eneo la Ruiru alifurushwa nchini siku ya Jumatano kufuatia tukio hilo. Katika ujumbe wake Murkomen alisema: “Najua tumekasirishwa na Liu Jiaqi kwa kutuita nyani.
Lakini hebu tuseme ukweli, ni wangapi kati yetu huwarushia wenzetu matusi mabaya kwa misingi kuwa wanatoka kabila tofauti? Ni wangapi kati yetu hutoa matusi mabaya kwa wenzetu kwa misingi ya kutofautiana kimawazo? Tuko na akina Lius Jiaqis wengi na wabaya zaidi miongoni mwetu.” Aliandika Murkomen. Kijana huyo wa Kichina ambaye anajulikana kwa lakabu ya ‘Juduge’ katika kampuni ya kuuza pikipiki ya Sonlink (K) Limited yenye makao yake mjini Ruiru, alinaswa kwenye kamera akimtusi mmoja wa wafanyakazi wa Kenya huku akivuka mpaka na kumtusi pia Rais Uhuru Kenyatta kwamba ni nyani. Kufuatia kusambaa video hiyo, Wakenya walionyesha kuchukizwa na matusi ya kijana huyo kupitia mitandao ya kijamii.