Upinzani Burundi wataka kufikia tamati mazungumzo ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47994-upinzani_burundi_wataka_kufikia_tamati_mazungumzo_ya_amani
Viongozi wa upinzani nchini Burundi wametaka mazungumzo ya amani yanayotazamiwa kufanyika baadaye mwezi huu kuwa ya mwisho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 09, 2018 02:51 UTC
  • Upinzani Burundi wataka kufikia tamati mazungumzo ya amani

Viongozi wa upinzani nchini Burundi wametaka mazungumzo ya amani yanayotazamiwa kufanyika baadaye mwezi huu kuwa ya mwisho.

Agathon Rwasa, kinara wa upinzani nchini humo ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge amesema, "Kikao kijacho kinapaswa kuwa cha mwisho na kinapaswa kujikita katika kuandaa mazingira ya kisiasa na ramani ya njia ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020."

Mashirika ya kijamii na kiraia hayatashirikishwa kwenye kikao kijacho cha mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo.

Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi, Michel Kafando kwa sasa yupo Bujumbura ambapo anakutana na kufanya mazungumzo na viongozi na wadau mbalimbali wa kisiasa na kijamii, kabla ya kufanyika mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Timu ya mazungumzo ya amani ya Burundi inayoongozwa na rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa ilipata ahueni baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwa hatogombea muhula mwingine, kwani kimya chake cha muda mrefu kuhusu jambo hilo kimekuwa kikikwamisha mazungumzo hayo ya amani mara kwa mara.

Burundi ilitumbukia katika machafuko ya kisiasa  mapema mwaka 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kugombea kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu; hatua ambayo ni kinyume na katiba ya nchi hiyo.