Serikali na wapinzani nchini Ivory Coast wazidi kuvutana kuhusu uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48245-serikali_na_wapinzani_nchini_ivory_coast_wazidi_kuvutana_kuhusu_uchaguzi
Mivutano baina ya serikali ya Ivory Coast na wapinzani wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kuhusiana na marekebisho katika Kamisheni Huru ya Uchaguzi imezidi kuongezeka.
(last modified 2025-11-18T07:21:20+00:00 )
Sep 19, 2018 14:36 UTC
  • Serikali na wapinzani nchini Ivory Coast wazidi kuvutana kuhusu uchaguzi

Mivutano baina ya serikali ya Ivory Coast na wapinzani wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kuhusiana na marekebisho katika Kamisheni Huru ya Uchaguzi imezidi kuongezeka.

Amadou Gon Coulibaly, Waziri Mkuu wa Ivory Coast amekataa takwa la wapinzani la kufanyiwa marekebisho Kamisheni Huru ya Uchaguzi kabla ya kufanyika uchaguzi ujao wa Mabaraza ya Miji na Serikali za Mitaa tarehe 13 ya mwezi ujao wa Oktoba na kutangaza kuwa, hakuna haja ya kufanyika marekebisho kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Waziri Mkuu wa Ivory Coast ameongeza kuwa, Kamisheni Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo iko tayari kwa ajili ya kuendesha zoezi la uchaguzi huo katika kiwango cha Mabaraza ya Miji na Serikali za Mitaa.

Amadou Gon Coulibaly, Waziri Mkuu wa Ivory Coast

Amadou Gon Coulibaly amebainisha kwamba, marekebisho ya kimsingi katika Kamisheni Huru ya Uchaguzi ya Ivory Coast yatafanyika kabla ya uchaguzi ujao wa Rais uliopangwa kufanyika nchini humo mwaka 2020.

Chama cha upinzani cha Demokrasi na kile cha Ivorian Popular Front cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Laurent Gbagbo vimetishia kwamba, vitauvuruga uchaguzi ujao wa Mabaraza ya Miji na Serikali za Mitaa endapo hakutafanyika marekebisho wanayotaka ndani ya Kamisheni Huru ya Uchaguzi.

Wakati huo huo, baadhi ya wagombea wa upinzani nchini Ivory Coast wamekuwa wakizungumzia suala la kuususia uchaguzi wa mwezi ujao wa Oktoba endapo matakwa yao ya kutaka Kamisheni Huru ya Uchaguzi ifanyiwe marekebisho hayatafanyiwa kazi.