Sep 25, 2018 14:10 UTC
  • Licha ya kufikiwa maafikiano ya kusitisha vita, mapigano yaanza tena Sudan Kusini

Mapigano kati ya vikosi vya jeshi la serikali ya Sudan Kusini na vya kundi kubwa zaidi la waasi yameanza tena kaskazini mwa nchi hiyo baada ya kupita wiki mbili tangu pande hizo mbili zisaini makubaliano ya usitishaji vita.

Msemaji wa jeshi Lul Roai Koang amesema: Wanachama wa kundi la waasi la Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Sudan Kusini Upinzanini (SPLA-IO) linaloongozwa na Riek Machar, makamu wa zamani wa rais wa nchi hiyo wamefanya operesheni kadhaa za kuwazingira askari wa serikali waliokuwa kwenye msafara katika maeneo ya Liech na Wau hapo jana.

Ameongeza kuwa mtu mmoja aliuawa na wengine tisa walijeruhiwa katika shambulio hilo la mizingiro ya barabarani. 

Rais Salva Kiir (kulia) na hasimu wake wa kisiasa Riek Machar

Hata hivyo naibu msemaji wa waasi wa SPLA-IO Lam Paul Gabriel amesema vikosi vya jeshi la serikali vilishambulia vituo vyao viwili katika eneo lenye utajiri wa mafuta la Unity hapo jana.

Gabriel aidha amesema vikosi vya jeshi la serikali ya Juba vilishambulia ngome mbili za waasi hao wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Sudan Kusini katika maeneo ya Mir Mir na Kuok jimboni Liech. 

Mapigano baina ya pande hizo mbili yameanza tena huku kila upande ukiulaumu upande wa pili, wakati hivi karibuni Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alisaini mkataba wa amani na makundi ya upinzani kwa madhumuni ya kuhitimisha vita vya ndani nchini humo. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Riek Machar atateuliwa tena kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo.

Mwaka 2011 Sudan Kusini ilijitenga na Sudan kwa uingiliaji na uungaji mkono wa Magharibi hususan Marekani na matokeo yake ni kwamba nchi hiyo changa zaidi duniani sasa imegeuka uwanja wa mapigano ya utumiaji silaha.../

Tags