Sep 26, 2018 13:46 UTC
  • Ripoti: Mapigano nchini Sudan Kusini yameua watu laki 4

Ripoti mpya inasema watu karibu laki nne wameuawa katika mapigano ya kikabila nchini Sudan Kusini.

Francesco Checchi, ofisa wa taasisi ya London School of Hygiene & Tropical Medicine iliyofanya utafiti huo amesema kuwa, hizi ndizo takwimu za kwanza sahihi kuwahi kutolewa kuhusu idadi ya watu waliouawa katika mapigano ya kikabila nchini humo, tokeo vita hivyo viripuke mwishoni mwa mwaka 2013 hadi sasa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo Jumatano, asilimia 50 ya watu 382,900 waliouawa kufikia sasa nchini Sudan Kusini ni wale walikuwa wamepata majeraha mabaya katika vita hivyo vya kikabila.

Naye Klem Ryan, mjumbe wa zamani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini amesema matokeo ya utafiti huo ni sahihi mno kuliko idadi ya watu 50,000 ambayo imekuwa ikitumika kwa muda mrefu.

Riek Machar na Rais Salva Kiir (kulia) wakisaini makubaliano ya amani

Hii ni katika hali ambayo, mapigano kati ya vikosi vya jeshi la serikali ya Sudan Kusini na vya kundi kubwa zaidi la waasi yameanza tena kaskazini mwa nchi hiyo baada ya kupita wiki mbili tangu Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini asaini mkataba wa amani na makundi ya upinzani kwa madhumuni ya kuhitimisha vita vya ndani nchini humo.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Riek Machar atateuliwa tena kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

 

Tags