Ubeberu wa Marekani haubakishi mtu, sasa ni zamu ya Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48466-ubeberu_wa_marekani_haubakishi_mtu_sasa_ni_zamu_ya_algeria
Msemaji wa ubalozi wa Marekani mjini Algiers amesema kuwa, Washington hivi sasa inachunguza uwezekano wa kuiwekea vikwazo Algeria kutokana na kununua silaha kutoka Russia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 29, 2018 11:14 UTC
  • Ubeberu wa Marekani haubakishi mtu, sasa ni zamu ya Algeria

Msemaji wa ubalozi wa Marekani mjini Algiers amesema kuwa, Washington hivi sasa inachunguza uwezekano wa kuiwekea vikwazo Algeria kutokana na kununua silaha kutoka Russia.

Kwa mujibu wa mtandao wa Intaneti wa TSE wa Algeria, LaSean Knox-Brown, msemaji wa ubalozi wa Marekani mjini Algiers amesema, kwa mujibu wa sheria za Marekani, nchi au watu wanaotia saini mikataba ya kununua zana za kijeshi kutoka Russia huwa wanawekewa vikwazo na Washington.

Msemaji huyo wa ubalozi wa Marekani nchni Algeria ameituhumu Russia kwamba inakiuka haki za binadamu na imefanya mashambulizi ya mitandao ya kompyuta huko Marekani, madai ambayo daima yamekuwa yakikanushwa na Moscow.

Kifaru cha T-90 cha Russia. Algeria ni mnunuzi mkubwa wa vifaru hiyo

 

Iwapo vikwazo vya Marekani vitatekelezwa dhidi ya Algeria, basi vitalenga kwa uchache katika sekta tano ambazo ni pamoja na kupigwa marufuku mabadilishano ya biashara na Marekani, kuzuiwa uingizaji na upelekaji wa bidhaa baina ya nchi hizo mbili pamoja na kukatwa uhusiano wa mfumo wa fedha kati ya Algeria na Marekani.

Algeria ni mnunuzi mkubwa wa vifaru aina ya T-90 pamoja na mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya makombora wa S-300 kutoka Russia.

Hivi karibuni Igor Baliaev, balozi wa Russia nchini Algeria alisema kuwa asilimia 50 ya silaha za Russia zinazouzwa barani Afrika huwa zinanunuliwa na Algeria.

Serikali ya Russia imeikosoa vikali Marekani kwa siasa zake za kibeberu za kuingilia mambo ya nchi nyingine ambayo hayana uhusiano wowote na Marekani na kusema kuwa zinalenga kukwamisha ushirikiano wa Russia na nchi nyingine ikiwemo Algeria.