Baraza la Usalama la UN lafanya ziara DRC kabla ya uchaguzi
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetuma ujumbe wake wa ngazi za juu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, miezi miwili kabla wananchi wa taifa hilo la Kiafrika waelekee katika masanduku ya kupiga kura kumchagua rais.
Karel Van Oosterom, balozi wa Uholanzi katika Umoja wa Mataifa ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Usalama ambao wanaitembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzia leo Alkhamisi hadi Jumatatu amesema, "Lengo la ziara hii ni kutathmini mazingira ya kabla ya uchaguzi ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo la kidemokrasia linafanyika katika anga ya amani, uwazi na haki."
Mbali na viongozi wa serikali na wakuu wa Tume ya Uchaguzi, wajumbe wa Baraza la Usalama la UN wanatazamiwa kukutana pia na kufanya mazungumzo na wadau wengine wa kisiasa na kijamii nchini humo.
Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Joseph Kabila wa DRC aliahidi mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba, serikali yake itahakikisha uchaguzi ujao wa nchi hiyo unafanyika vizuri na katika mazingira huru na ya haki.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Desemba 23 mwaka huu, huku manung'uniko ya wapinzani baada ya baadhi ya wagombea wao kuzuiwa kushiriki uchaguzi huo, yakiendelea kusikika.
Moise Katumbi, mwanasiasa wa upinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye kwa sasa yuko uhamishoni nchini Ubelgiji hivi karibuni alitadharisha kuwa, matokeo ya uchaguzi wa rais utakaofanyika nchini humo mwishoni mwa mwaka huu huenda yakavuruga amani na uthabiti sio tu katika nchi hiyo bali kote barani Afrika.