Amnesty: Watu 52 wameaga dunia wakiwa kizuizini Madagascar
(last modified Tue, 23 Oct 2018 13:30:51 GMT )
Oct 23, 2018 13:30 UTC
  • Amnesty: Watu 52 wameaga dunia wakiwa kizuizini Madagascar

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema watu 52 walifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha wakiwa korokoroni wakisubiri kesi zao mwaka jana 2017 nchini Madagascar.

Ripoti iliyotolewa leo Jumanne na Amnesty International yenye anwani inayosema "Kuadhibiwa Kutokana na Umaskini" imesema asilimia 55 ya wafungwa (wafungwa 11,000) katika magereza ya kisiwa hicho kilichoko katika Bahari Hindi wangali wanasubiri kesi zao tangu Oktoba mwaka jana, licha ya kuwa baadhi ya mashtaka yanayowakabili ni madogo.

Deprose Muchena, Mkurugenzi wa eneo la Kusini mwa Afrika wa Amnesty International amesema mfumo wa mahakama na sheria nchini Madagascar unapaswa kurekebishwa kwani wafungwa wengi wanapitia kipindi kigumu wakiwa kizuizini kabla ya kesi zao kuanza kusikilizwa.

Ramani ya Madagascar

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu kwa upande wake imesema nusu ya wafungwa katika kisiwa hicho wanaandamwa na utapiamlo wa wastani na wa kiwango cha juu.

Itakumbukwa kuwa, Mei mwaka 2016, makumi ya wafungwa walitoroka jela ya Tuléar, kusini magharibi mwa nchi hiyo ambayo asilimia 76 ya wakazi wake wanaishi katika hali mbaya ya umaskini.