Mripuko wa bomu Sinai, Misri waua wafanyakazi watatu
Wafanyakazi watatu raia wa Misri wameuawa katika shambulizi la bomu lililotokea leo Alkhamisi katika eneo linalokumbwa na misukosuko na ukosefu wa usalama la Rasi ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.
Maafisa usalama nchini humo wamethibitisha kutokea tukio hilo na kufafanua kuwa, bomu la kutegwa ardhini liliripuka na kuwaua wafanyakazi watatu waliokuwa wamepewa kandarasi ya kujenga ukuta wa usalama katika mji wa Arish, kaskazini mwa nchi.
Habari zaidi zinasema kuwa, wafanyakazi wengine 10 wamejeruhiwa katika mripuko huo ambao unahusishwa na genge lenye mfungamano na magaidi wakufurishaji wa ISIS (Daesh).
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya Bunge la Misri kurefusha muda wa hali ya hatari kwa miezi mingine mitatu na hivyo kurefusha nguvu ya serikali ya kutumia madaraka maalumu kuelekea mwaka 2019.
Kwa mara ya kwanza Misri ilianza kutekeleza hali ya hatari nchini humo mwezi Aprili mwaka 2017 baada ya kutokea milipuko katika makanisa mawili na kuuawa watu wasiopungua 45, na imekuwa ikirefushwa kwa miezi mitatu.
Mwezi Februari mwaka huu jeshi la Misri lilianzisha oparesheni kubwa ya kuwasaka wanachama wa magenge ya kigaidi haswa katika Peninsula ya Sinai, kaskazini mwa nchi.