Nov 01, 2018 16:20 UTC
  • Wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa Boko Haram wameuwa watu 15 Nigeria

Wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram wamewauwa watu wasiopungua 15 katika shambulio dhidi ya vijiji vilivyoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo jana jioni.

Vijiji hivyo vinapatikana katika vitongoji vya mji wa Maiduguri ambacho ni kitovu cha mapambano ya serikali kaskazini mashariki mwa Nigeria na makao makuu ya oparesheni za kuliangamiza kundi la Boko Haram na la ISWA lenye mfungamano na Boko Haram  huko magharibi mwa Afrika. Kundi hilo linaendesha hujuma kwa karibu muongo mmoja sasa. Licha ya serikali ya Nigeria kutangaza mwishoni mwa mwaka 2015 kuwa Boko Haram limesambaratishwa kwa kiasi kikubwa, lakini kundi hilo lingali lina uwezo wa kufanya mashambulizi katika mji wa Maiduguri, maeneo ya karibu yake na katika maeneo mengi ya kaskazini mashariki mwa Nigeria.  

Mji wa Maiduguri huko kaskazini mashariki mwa Nigeria

Katika kijiji cha Kofa ripota wa shirika la habari la Reuters amehesabu miiili ya watu watano walioungua ndani ya mabaki ya nyumba yao. Wakati huo huo kiongozi wa kijiji cha karibu cha Dalori amesema kuwa mtu mmoja ameuawa katika kambi ya wakimbizi huku wakazi wawili wa eneo la Bulabrin wakiripotiwa kuaga dunia katika eneo hilo.

 

 

 

 

Tags