Nov 09, 2018 07:58 UTC
  • UN:Hatua mpya zinafanikisha vita dhidi ya Ebola DRC

Hatua mpya za kukabiliana na changamoto za vita dhidi ya mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC zinazaa matunda ingawa mlipuko huo bado unasalia kuwa hatari.

Hayo yameelezwa Alhamisi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya duniani , WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus na Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix walipozungumza kwa pamoja na waandishi wa habari baada ya kuzuru maeneo mbalimbali ya Beni Mashariki mwa DRC ambako ndio kitovu cha mlipuko wa Ebola.

Maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wamepata fursa ya kukutana na wahudumu wa afya , wawakilishi wa asasi za kiraia, walinda amani na uongozi wa eneo hilo na kupongeza juhudi kubwa zinzofanywa na wahudumu wa afya na wadau wengine katika vita dhidi ya kusambaa kwa Ebola. Dkt Tedros amewaeleza waandishi wa habari kwamba kuna changamoto lakini pia kuna mafanikio mengi  hasa mafanikio katika kuzuia usambaaji katika eneo la Mangina, Oicha, Makeke na Komanda. Aidha amesema ukweli kwamba Ebola haijasambaa katika majimbo mengi na nchi jirani ni ushahidi tosha wa kazi kubwa inayofanywa na washirika wote.Hata hivyo amesema changamoto kubwa katika juhudi hizo ni usalama.

Chanjo ya majaribio ya Ebola

Tangu mlipuko mpya wa Ebola ulipozuka mwezi Agosti kumekuwa na visa 308 na vifo 191, na takribani nusu ya visa hivyo vimekuwa Beni mji ulio na watu laki 8. Na mlipuko wa sasa ni mlipuko wa 10 katika historia ya nchi hiyo na uko mbioni kuvunja rekodi ya mlipuko mkubwa kabisa uliopita mjini Yambuku mwaka 1976 ambapo kulikuwa na visa 318 na vifo 280.

Mpaka sasa watu 27,000 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola na kila mmoja amepata moja ya dawa nne mpya za majaribio kitu ambacho hakijawahi kufanyika hapo kabla.

 

Tags