Makumi ya wahajiri wajifungia kwenye kontena Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49517-makumi_ya_wahajiri_wajifungia_kwenye_kontena_libya
Makumi ya wahajiri wamejifungia kwenye shehena iliyoko ndani ya meli moja katika mji bandari wa Misrata kwa muda wa siku tano sasa baada ya kuokolewa, wakisisitiza kuwa Libya ni nchi hatari sana kwao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 15, 2018 00:03 UTC
  • Makumi ya wahajiri wajifungia kwenye kontena Libya

Makumi ya wahajiri wamejifungia kwenye shehena iliyoko ndani ya meli moja katika mji bandari wa Misrata kwa muda wa siku tano sasa baada ya kuokolewa, wakisisitiza kuwa Libya ni nchi hatari sana kwao.

Mmoja wa wahajiri hao 93 raia wa Sudan Kusini aliliambia shirika la habari la Associated Press jana Jumatano kuwa, katu hatakubali kurejeshwa nchini Libya, na bora afe akiwa katika jitihada za kuelekea barani Ulaya. Raia huyo wa Sudan Kusini amenukuliwa na AP akisema kuwa, "Hatutaki kwenda Libya, kaka yangu alifia jela huko Libya. Siondoki hapa, labda mje mnichukue nikiwa maiti."

Wahajiri hao waliokolewa Ijumaa usiku na Meli ya Nivin iliyokuwa imesheheni magari katika bahari ya Mediterania, wakiwa katika safari hatarishi ya kuelekea Ulaya.

Wahajiri wawili hata hivyo wamekubali kuondoka kwenye shehena hiyo ambayo kwa sasa inalindwa na Gadi ya Pwani ya Libya, huku wenzao 93 wakiwemo wanawake na watoto wakiendelea kusota ndani yake.

Baadhi ya wahajiri wakizama katika bahari ya Medittaraenia

Itakumbukwa kuwa, wahajiri wanane wakiwemo watoto sita walipoteza maisha baada ya kuishiwa na hewa wakiwa ndani ya kasha la kusafirishia mizigo katika mji wa Zuwara ulioko katika pwani ya magharibi mwa Libya mwezi Julai mwaka huu.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa ya Wahajiri IOM, hivi sasa kuna zaidi ya wahamiaji haramu laki saba kutoka nchi 40 tofauti nchini Libya, ambapo asilimia 63 ya wahamiaji haramu hao wanatoka katika nchi za Afrika zilizoko chini ya jangwa la Sahara.