Wafanyakazi wa umma waandamana wakitaka nyongeza ya mishahara Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49695-wafanyakazi_wa_umma_waandamana_wakitaka_nyongeza_ya_mishahara_tunisia
Maelfu ya watumishi wa umma nchini Tunisia jana Alkhamisi walimiminika mabarabarani kushiriki maandamano ya kushinikiza nyongeza ya mishahara.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 23, 2018 04:16 UTC
  • Wafanyakazi wa umma waandamana wakitaka nyongeza ya mishahara Tunisia

Maelfu ya watumishi wa umma nchini Tunisia jana Alkhamisi walimiminika mabarabarani kushiriki maandamano ya kushinikiza nyongeza ya mishahara.

Watu zaidi ya elfu tatu aghalabu yao wakiwa walimu, madaktari, wahadhiri na wafanyakazi wa wizara walikusanyika nje ya Bunge la nchi hiyo mjini Tunis, wakiitaka serikali ijiuzulu kwa kushindwa kutekeleza matakwa yao. 

Maandamano hayo yaliitishwa na Muungano Mkuu wa Wafanyakazi Tunisia  (UGTT), baada ya wakuu wake kutoafikiana na serikali katika mazungumzo kuhusu mgogoro huo.

Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe zinazosema: Tunisia sio ya kuuzwa; Kazi! Uhuru! Hadhi ya Kitaifa! 

Hivi karibuni pia, wanafunzi wanaosomea taaluma ya udaktari nchini Tunisia walifanya maandamano nje ya ofisi ya Wizara ya Afya katika mji mkuu Tunis, wakishinikiza kutekelezewa matakwa yao.

Wafanyakazi wa umma wamekuwa wakiandamana mara kwa mara Tunisia, tokea Msimu wa Machipuo wa 2011

Aidha mapema mwaka huu, mamia ya watu walitiwa mbaroni mjini Tunis kwa kushiriki maandamano dhidi ya serikali ya kulalamikia ongezeko la bei za bidhaa na kodi.

Serikali ya Tunisia inatekeleza sera za kubana matumizi kiuchumi kutokana na kushuka mno thamani ya sarafu ya nchi hiyo na kukabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti.