Waislamu Nigeria waendelea kuandamana kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49837-waislamu_nigeria_waendelea_kuandamana_kutaka_sheikh_zakzaky_aachiliwe_huru
Wananchi Waislamu wa Nigeria wamefanya maandamano ya kutaka kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 28, 2018 23:40 UTC
  • Waislamu Nigeria waendelea kuandamana kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru

Wananchi Waislamu wa Nigeria wamefanya maandamano ya kutaka kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.

Kanali ya televisheni ya Al-Alam imeripoti kuwa, kwa mara nyengine, Waislamu wa Nigeria wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja, wakiitaka serikali imwachie huru kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo, Sheikh Zakzaky, ambaye amewekwa kizuizini kwa zaidi ya mwaka wa tatu sasa pasi na kuthibitishwa tuhuma zozote dhidi yake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika maandamano yao hayo, Waislamu hao walitoa sha'ar na miito kadhaa ya shime ya kumuunga mkono Sheikh Zakzaky.

Sheikh Ibrahim Zakzaky

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walikamatwa na kuwekwa kizuizini tarehe 13 Desemba 2015, wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kufanya hujuma dhidi ya Hussainiyyah ya mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo.

Mnamo mwezi Desemba 2016, Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa hukumu ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiwe huru mara moja, sambamba na kulitaka jeshi na vyombo vya usalama viilipe familia yake fidia ya dola laki moja na nusu, lakini si tu vimekaidi kutekeleza hukumu hiyo ya mahakama lakini vimeendelea pia kumweka kizuizini kiongozi huyo wa kidini pamoja na mkewe.../